MBOWE AMBANA MAJALIWA KUHUSU MAAZIMIO YA BUNGE

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amemuuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu kutokutekelezwa maazimio ya Bunge ikiwemo Escrow, Tokomeza na mabilioni ya Uswiss.
Akijibu swali hilo Majaliwa alimuhakikishia Mbowe kuwa Serikali inaheshimu muhimili wa Bunge na kuthamini maamuzi yake.

Amesema kunahitajika uchunguzi wa kina na yapo ambayo yana umuhimu wa kuletwa bungeni hivyo uchunguzi wa Serikali utakapokamilika yatawasilishwa bungeni.

Advertisements

SHILOLE ASHINDWA KUFIKA MAHAKAMANI KUTOA USHAHIDI 

Msanii wa muziki wa kizazi wa Bongo Fleva na filamu, nchini Zuwena Mohamed maarufu kama  Shilole ameshindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi katika kesi ya matumizi mabaya ya mtandao kwa kuwa anaumwa.
Leo (Jumatano) Shilole alipaswa kutoa ushahidi katika kesi hiyo inayomkabili mwanafunzi wa Chuo cha Bandari, Thomas Lucas (20) inayosikilizwa mbele ya Hakimu Boniface Lyamwike.

Katika kesi hiyo, Lucas anakabiliwa na shtaka la mtandao kwa kumkashfu Shilole kupitia kwenye mtandao wa Instagram.

Inadaiwa  kuwa mshtakiwa huyo alifanya hivyo wakati akijiua ni kosa na kinyume na kifungu cha 16 cha sheria ya mtandao namba 14 ya 2016.

Hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 17,2017 ambapo itaendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

MBUNGE ATAKA KUTUMIA KISWAHILI UCHAGUZI EALA 

Baadhi ya wabunge wameibua hoja ya kutaka Kiswahili kitumike kuwauliza maswali wagombea wa Chadema wanaojinadi kuwania nafasi ya ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala). 
Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Musukuma’ baada ya kupewa ruhusa na Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema kwa kuwa sifa ya kuchaguliwa kuwa mbunge nchini ni kujua kusoma na kuandika, hivyo Kiswahili kitumike kuwauliza maswali.

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililla amesema mbunge anaweza kuuliza swali kwa Kiswahili lakini mgombea atapaswa kujibu wa Kiingereza.

Baada ya jibu hilo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amesema iwapo swali litaulizwa kwa Kiswahili, basi atafutwe wa kutafsiri kwa kuwa hata majibu hayo hatayaelewa.

MKURUGENZI WA BREAK POINT AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUTOTUMIA MASHINE YA EFD

Mkurugenzi wa Hotel ya Break Point, David Machumu amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya Kinondoni akituhumiwa kwa mashtaka matatu likiwemo la kushindwa kutoa risiti katika mashine za elektroniki (EFDs). 
Akisoma  hati ya mashtaka  Wakili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) wa  Wilaya ya Kinondoni, Juliana Ezekiel amedai kuwa  tukio hilo lilitokea Oktoba 8, mwaka 2016 katika hoteli hiyo iliyopo Kinondoni.

Wakili Ezekiel amedai kuwa mtuhumiwa kwa makusudi na bila sababu alipokea Sh12,000 kutoka kwa mteja ajili ya vinywaji bila ya kutumia mashine za EFDs ambapo kufanya hivyo ni kosa kinyume cha sheria ya kodi.

SH 30 BILIONI KULIPA FIDIA KWA WAKAZI WA KIPUNGUNI

Serikali imetenga Sh30 bilioni (30) katika mwaka wa fedha 2017/2018 ili kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi wa Kipunguni wanaopisha upanuzi wa uwanja wa ndege.
Hayo yamesemwa leo (Jumanne) bungeni  na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani   wakati akijibu swali la Mbunge wa Segerea , Bonnah Kaluwa.

“Ni kweli Serikali ilifanya uthamini wa mali za wananchi ili kupisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Dar es Salaam mwishoni wa miaka ya 90 ambapo maeneo yaliyoainishwa kwa ajili ya upanuzi huo ni Kipawa,Kigilagila na Kipunguni”, amesema.

Ngonyani amesema kuwa kutokana na gharama za fidia na uhaba wa fedha Serikali imekuwa ikilipa fidia kwa wakazi hao kwa awamu.

MKOA MPYA WA KIPOLISI KUANZISHWA RUFIJI 

Serikali imetangaza kuanzisha mkoa mpya wa kipolisi katika wilaya za Mkuranga, Kibiti,  Rufiji na Mafia ili kuimarisha usalama katika maeneo hayo.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amelieleza Bunge leo (Jumanne) katika hotuba yake ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2017/18.
Nchemba amesema mkoa huo utaitwa Mkoa wa Kipolisi Rufiji.
Kibiti kumekuwa na matukio mbambali ya mauaji ambayo yamegharimu maisha ya baadhi ya wananchi.

LEMA,MSIGWA WALIANZISHA BUNGENI 

Wabunge wawili wa Chadema, Peter Msigwa wa Iringa Mjini na Godbless Lema wa Arusha Mjini wameomba mwongozo wa Spika kuhusu ubaguzi wa kisiasa uliotokea kwenye msiba mjini Arusha Jumatatu.
Jana Jumatatu jijini Arusha ilikuwa inaagwa  miili ya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa Shule ya Lucky Vincent waliopoteza maisha katika ajali ya gari.

Wa kwanza kusimama alikuwa Msigwa ambaye amehoji kama ni haki kutowapa fursa Meya wa Arusha, Calist Lazaro na Mbunge wa jimbo hilo, Lema kutoa salamu za rambirambi.

Lema kwa upande wake amesema hata magari mawili ya kubeba wagonjwa yaliyotolewa na yeye na mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari yaliondolewa kwa sababu yana majina yao.

Amesema ni kwa sababu walimheshimu makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, vinginevyo mambo kama hayo huwa hayatokei mbele yao.

Mwenyekiti wa Bunge  Najma Giga amesema atatoa mwongozo huo baadaye.

RAIS ZUMA KUTUA NCHINI NA WAFANYABIASHARA 80

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma anatarajiwa kufanya ziara ya siku tatu nchini kuanzia Mei 10 – 12, mwaka huu akiwa ameambatana na mawaziri sita na zaidi ya wafanyabiashara 80.
Katika ziara hiyo, Rais Zuma atakuwa na mazungumzo na mwenyeji wake, Rais John Magufuli na baadaye kufanya mazungumzo ya pamoja kati ya ujumbe wa Afrika Kusini na ujumbe wa Tanzania.

Akizungumzia ziara hiyo leo, Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustino Mahiga amesema Serikali za Tanzania na Afrika Kusini zitatiliana saini zaidi ya mikataba 10 kwenye sekta za biashara, uwekezaji, miundombinu, utalii, elimu, afya na nishati.

“Kwa kuanzia tutatiliana saini mkataba wa utunzaji wa mazingira (biodiversity), uchukuzi na nishati. Hiyo mingine bado inaandaliwa, itasainiwa baadaye,” amesema Dk Mahiga.

Waziri huyo amesema nchi za Afrika Kusini na Tanzania zimeamua kutumia uhusiano wa kihistoria kama fursa ya kuanzisha uhusiano mpya wa kiuchumi kwa kuongeza uwekezaji na biashara.

Amesema uwekezaji wa Afrika Kusini hapa nchini umezidi kuongezeka kutoka Dola za Marekani 803 milioni mpaka kufikia Dola bilioni 2.2 mwaka 2016 na kuifanya nchi hiyo kuwa ya pili kwa kuwa na uwekezaji mkubwa nchini baada ya Uingereza.

“Uwekezaji wa Watanzania nchini Afrika Kusini bado ni duni, zipo fursa nyingi kule lakini hazijatumika vizuri. Hii ni nafasi kwa wafanyabiashara wetu kuzungumza na wenzao wa Afrika Kusini,” amesema.

Katika ziara hiyo, Zuma atashiriki mkutano wa wafanyabiashara, atazindua jengo la Ubalozi wa Afrika Kusini na kutembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

WABUNGE WATOA POSHO ZAO KUOMBOLEZA VIFO VYA WANAFUNZI

Wabunge wametoa posho ya siku moja ya kikao kwa ajili ya rambirambi ya vifo vya wanafunzi, walimu na dereva wa Shule ya Lucky Vincent ya jijini Arusha.
Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema amepata ushauri kutoka kambi zote mbili bungeni kutoa posho yao ya siku moja, fedha ambazo zitagawanywa kwa usawa kwa ndugu wa marehemu wa ajali hiyo.

Kutokana na ushauri huo, ameomba wabunge waamue kuhusu suala hilo jambo ambalo lilikubaliwa na wote.

Kabla ya kuanza kwa shughuli za Bunge leo, wabunge walisimama kwa dakika moja kuwakumbuka waliofariki dunia katika ajali hiyo.

Wanafunzi 33, walimu wawili na dereva mmoja walikufa katika ajali iliyotokea Jumamosi iliyopita eneo la Rotya wilayani Karatu wakati wanafunzi wa shule hiyo iliyopo Olasiti jijini Arusha wakienda kufanya mtihani wa ujirani mwema katika Shule ya Tumaini Junior Acadamy.

tanzaniayetu