POLISI WAZUIA MKUTANO WA CUF TANGA 

Mgogoro  uliopo ndani ya CUF umeendelea kukiletea  chama hicho athari baada ya ziara ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya chama hicho Taifa, Julius Mtatiro jijini Tanga kuzuiwa na jeshi la polisi.
Mtatiro  aliwasili jijini Tanga jana jioni kwa lengo la kufanya vikao vya ndani pamoja na kufungua matawi  kazi ambayo ilikuwa aifanye leo na kesho.

Mwenyekiti wa CUF ,Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe amesema licha ya

kwamba hadi jana jioni walikuwa na barua kutoka jeshi la polisi ya

kuwaruhusu kuendelea na ziara ya Mtatiro lakini leo saa 3.00 asubuhiwalizuiwa.

“Tulipopewa taarifa ya kuzuiwa, tuliamua kwenda kwa OCD Tanga

tukiambatana na mheshimiwa Mtatiro  kupata maelezo ya kwa nini tuzuiwe ndipo tukaambiwa Magdalena Sakaya ametuma barua ya kuzuia mikutano hiyo kwa madai kwamba hana taarifa,”amesema Jumbe.

Mwenyekiti  huyo alieleza kushangazwa kwake na kitendo cha jeshi la

polisi kufanyia kazi maelekezo ya Sakaya huku akisisitiza kwamba CUF

Tanga haimtambui  kwa sababu alishafukuzwa uanachama.

“Magdalena Sakaya na Profesa Ibrahim Lipumba sisi Tanga hatuwatambui

kwa sababu si wanachama wa CUF, hao ni viongozi wa Msajili wa Vyama

vya Siasa, watambue kwamba njama zao za kuiua CUF hazitafanikiwa

kamwe,” amesema Jumbe.

Amesema Julias Mtatiro alikuwa amepangiwa  kukutana na viongozi wa

kamati ya utendaji ya Wilaya ya Tanga, madiwani, wabunge, kufungua matawi

ya Kata ya Duga, Masiwani Shamba, Masiwani, Mabawa, Magaoni, Mnyanjani, Pongwe na Kwanjeka.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amesema

wamezuia ziara hiyo kufuatia jeshi la polisi kupokea  barua mbili

tofauti zenye kupingana jambo lililoashiria kuwa kusingekuwa na amani.

Leave a comment