KIZIMBANI KWA USAFIRISHAJI HARAMU WA WATU 11

Raia wa Kenya, Samson Mbaria Pirias maarufu kama Babaa(38) na raia wa Tanzania, Lohelo Boniphace Mwabulanga maarufu Diblo(43) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kusafirisha raia 11 kutoka Kenya kwenda Afrika Kusini kuwafanyisha kazi kinguvu.
Akisoma hati ya mashtaka,Wakili wa Serikali, Elia Athanas amedai kuwa washtakiwa hao walifanya kosa kinyume na kifungu cha 4(1)(a) na (1)(2)(c) na 4 cha sheria ya kusarifisha binadamu sura ya sita ya 2008.

Amedai kuwa Februari 28 ,2017 huko Chanika wilaya ya Ilala washtakiwa hao walikamatwa wakiwasafirisha watu hao 11 kutoka Kenya kwenda Afrika Kusini kwa lengo la kuwafanyisha kazi kinguvu.

Watu hao ni Dhaha Maliya All, Hassen Gales Omar, Ahmed Lobiso Abdi,Dhawil Ayantu Duri, Omar Yahye Mohammed, Hikma Ibrahim Omar, Istahil Ali Shukri, Rashid Omar Yusuf,Abdul Khalid Asiis, Abdulah Sartu na Hassen Guled Omar.

Baada ya kusomewa shtaka hilo washtakiwa walikana na wamepelekwa rumande kwa sababu shtaka linalowakabili la kusafirisha binadamu ni moja kati ya mashtaka yasiyo na dhamana.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na wakaomba ipangiwe tarehe ya kutajwa.

Hakimu Mwambapa aliiahirisha hadi Mei 17,2017 kwa ajili ya kutajwa kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Leave a comment