KIZIMBANI KWA USAFIRISHAJI HARAMU WA WATU 11

Raia wa Kenya, Samson Mbaria Pirias maarufu kama Babaa(38) na raia wa Tanzania, Lohelo Boniphace Mwabulanga maarufu Diblo(43) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kusafirisha raia 11 kutoka Kenya kwenda Afrika Kusini kuwafanyisha kazi kinguvu.
Akisoma hati ya mashtaka,Wakili wa Serikali, Elia Athanas amedai kuwa washtakiwa hao walifanya kosa kinyume na kifungu cha 4(1)(a) na (1)(2)(c) na 4 cha sheria ya kusarifisha binadamu sura ya sita ya 2008.

Amedai kuwa Februari 28 ,2017 huko Chanika wilaya ya Ilala washtakiwa hao walikamatwa wakiwasafirisha watu hao 11 kutoka Kenya kwenda Afrika Kusini kwa lengo la kuwafanyisha kazi kinguvu.

Watu hao ni Dhaha Maliya All, Hassen Gales Omar, Ahmed Lobiso Abdi,Dhawil Ayantu Duri, Omar Yahye Mohammed, Hikma Ibrahim Omar, Istahil Ali Shukri, Rashid Omar Yusuf,Abdul Khalid Asiis, Abdulah Sartu na Hassen Guled Omar.

Baada ya kusomewa shtaka hilo washtakiwa walikana na wamepelekwa rumande kwa sababu shtaka linalowakabili la kusafirisha binadamu ni moja kati ya mashtaka yasiyo na dhamana.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na wakaomba ipangiwe tarehe ya kutajwa.

Hakimu Mwambapa aliiahirisha hadi Mei 17,2017 kwa ajili ya kutajwa kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

KAMANDA SIMON SIRRO ATAJA WANAFUNZI WAWILI WALIOFARIKI KWENYE AJALI DAR ASUBUHI 

Watu wawili wamepoteza maisha na wengine 24 kujeruhiwa kutokana na ajali iliyotokea leo (Jumatano) eneo la Superdoll Barabara ya Mwalimui Nyerere jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema ajali hiyo ya uso kwa uso  imehusisha lori aina ya Scania na Bus Eicher lenye lililokuwa likitokea Gongo la Mboto.

Sirro amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Itlam Athuman (mwanafunzi wa shule ya Sekondari Msimbazi kidato cha kwanza) na Sakina Imamu  (Mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya Sekondari Mchikichinj).  

“Majeruhi wametibiwa katika Hospitali ya Temeke na baadhi yao wameruhusiwa wamebakia watatu tu. Jeshi la polisi linamshikilia dereva wa lori hilo kwani ajali hiyo imesababishwa na uzembe wake wa kuingia barabarani bila kuchukua tahadhari,” anasema Sirro

TELEVISHENI,REDIO KUSOMA VICHWA VYA HABARI TU KWENYE MAGAZETI-DK MWAKYEMBE

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amezitaka Televisheni na Redio kuanzia kesho kusoma vichwa vya habari vya magazeti tu ili kuwavutia wasomaji kununua magazeti kwa habari kamili.
Dk Mwakyembe amesema hayo leo jijini Mwanza katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari nchini ambapo pia amesema ataendelea kutetea na kulinda haki za waandishi wa habari huku akiwahakikishia ulinzi waandishi wa habari za uchunguzi.

Pamoja na mambo mengine Dk Mwakyembe amehakikisha kuwepo kwa ushirikiano wa kutosha kwa wamiliki wa vyombo vya habari  na kwamba ameagiza idara ya mawasiliano kutengeneza mawasiliano ya kudumu na wawe wanakutana angalau mara moja kwa mwezi kujadili udhaifu unaoweza kujitokeza na kuchukua hatua lengo ni kuwekana  sawa.