WABUNGE WAGEUZWA ATM KWA KUJITAKIA 

Wakati wabunge wakionyesha kukerwa na kugeuzwa ATM majimboni kwao, Katibu wa Spika, Saidi Yakubu amewaeleza kuwa wao ndio chanzo hivyo wakiamua tatizo hilo litakwisha.
Yakubu alikuwa akijibu hoja mbalimbali za wabunge zilizotolewa walipokuwa wakichangia kwenye semina kuhusu wajibu wa wabunge wanachama wa mabunge ya nchi za Jumuiya ya Madola (CPA) katika kufanikisha maendeleo endelevu.

Alisema wabunge wamekuwa ni sehemu ya tatizo hilo kwani mwaka 2008 waliendesha mradi wa kutoa elimu kwa umma na walikwenda katika mikoa mbalimbali ikiwamo Ruvuma lengo likiwa ni kuwaeleza majukumu ya mbunge kwa wapigakura.

“Tuliwaeleza wananchi kuwa kazi ya mbunge sio kulipa ada, bali ni kushawishi Serikali kuangalia upya ada kama gharama ni kubwa,” alisema.

Hata hivyo, alisema baada ya maelezo hayo alisimama diwani mmoja na kusema mtoa mada amewadanganya mbona mbunge (aliyekuwapo eneo hilo) alimuahidi kuwa akishinda ubunge atampatia fedha.

Alisema tabia ya wabunge kutoa fedha kwa wananchi sio kwa Tanzania tu, bali imejitokeza kwa nchi nyingine ikiwamo India, Australia (baadhi ya maeneo) na kuwashauri kuungana kulimaliza tatizo hilo.

Katibu huyo alisema wabunge wana jukumu la kulitatua tatizo hilo kwa sababu fedha wanazopata ni ndogo na hawawezi kutoa kwa mtu mmoja mmoja.

Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alisema katika nchi mbalimbali ikiwamo Kenya ofisi ya mbunge ni taasisi tofauti na Tanzania ambapo mbunge ni ATM. “Mbunge wa Tanzania ni ATM, ni kabenki kadogo pamoja na ufinyu wa fedha anazopata lakini kila mwezi anakatwa Sh1.2 milioni na mafao yake ya mwisho (baada ya miaka mitano) pia anakatwa, ukiagiza gari pia unakatwa,” alisema.

Alisema kukiwa na harambee mbunge anaitwa kama mgeni rasmi na kutakiwa kuchangia wakati mwingine Sh70 milioni na kuhoji fedha hizo zinatoka wapi.

Akizungumzia demokrasia na uhuru wa mawazo, Waitara alisema utakuta mbunge ana jambo zuri lakini anashindwa kulizungumzia kwa sababu ya itikadi ya vyama.

Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema Tume ya Utumishi wa Bunge imelifanyia kazi suala la bima ya maisha ya afya kwa wabunge ambalo lipo kisheria lakini hawajahi kupata haki hiyo

Alisema Tume ya Utumishi wa Bunge imuite Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama kumwelezea kuhusu jambo hilo ambalo liko kisheria lakini hakulifanyia kazi.

“Wabunge hawana bima ya maisha ya afya ingawa ipo kisheria na wengi wamekufa na kupata ulemavu,” alisema.

Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), Naghenjwa Kaboyoka alisema kamati za za Bunge hazina ofisi ambazo zinawawezesha kukaa na kupanga mipango yao. Pia alisema wabunge wameendelea kuchangia kichama na hivyo kushindwa kuitikisa Serikali hata kama wakiwa na msimamo katika jambo lenye masilahi kwa wananchi.

Mbunge wa Songwe (CCM) Philipo Mulugo alitaka mchanganuo wa mishahara, marupurupu na posho ya jinsi yanavyolipwa mabunge mengine ya Jumuiya ya Madola ili walinganishe na ya kwao.

Akijibu hoja za wabunge, Yakubu alisema nia yake ilikuwa ni kuchokoza mada lakini utafiti wa mafao umefanyika katika mabunge ya jumuia hiyo na kwamba kuupata hapo walipo ni ngumu.

Advertisements

MVUA YATENGANISHA KATI YA BUKOBA NA MWANZA MADEREVA WATUMIA NJIA MBADALA

Barabara hiyo imekatika leo (Ijumaa) saa 11:00 alfajiri kutokana na mvua iliyonyesha usiku kucha na kusababisha maji kujaa kwenye karavati.
Mvua imesababisha barabara kuu ya Mwanza -Bukoba kukatika eneo la Kemondo, hivyo magari ya abiria na mizigo kuzunguka Kyetema kupitia Katerero kutokea Muleba.

Barabara hiyo imekatika leo (Ijumaa) saa 11:00 alfajiri kutokana na mvua iliyonyesha usiku kucha na kusababisha maji kujaa kwenye karavati.

Kutokana na hali hiyo wananchi na hasa wafanyabiashara wa eneo la Kemondo wameshindwa kuendelea na shughuli zao kwa kukosa mawasiliano.

Wakazi wa Kemondo wamesema wanafunzi wamekatisha masomo baada ya kukosa eneo la kupita.

Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Kagera, Andrew Kasamwa amesema watumiaji wa barabara hiyo wanatumia njia mbadala kwa kupita Katerero mzunguko wa umbali wa takriban kilomita 10.

Amesema jitihada zinafanywa kukarabati eneo hilo ili kurejesha mawasiliano.

TRUMP ASISITIZA HACHUNGUZWI NA FBI

Rais wa Marekani Donald Trump amesema hachunguzwi  na mtu yeyote wala shirika la ujasusi la FBI halimchunguzi. Hiyo ni baada ya kumfuta kazi mkurugenzi wa shirika la FBI.
Akizungumza na chombo cha habari cha NBC jana, Trump alisema  kwamba ilikuwa uamuzi wake pekee kumsimamisha kazi James Comey.

Comey alikuwa akiongoza uchunguzi kuhusu madai ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani uliokamilika mbali na uwezekano kwamba kulikuwa na mawasiliano kati ya maofisa wa Trump na Urusi wakati wa kampeni.

Trump ameutaja uchunguzi huo kuwa unafiki mkubwa madai yaliyopingwa na mrithi wa Comey.

Katika mahojiano yake ya kwanza tangu alipomfuta kazi mkurugenzi huyo, Trump aliiambia NBC siku ya Alhamisi kwamba alimuuliza Comey iwapo alikuwa akimchunguza.

“Nilimwambia iwapo inawezekana unaweza kuniambia, Je Ninachunguzwa? Aliniambia, huchunguzwi.” alisema Trump

WASANII WAMJIA JUU MWAKYEMBE KUHUSU KUJIHUSISHA NA SIASA 

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amejipalia makaa.
Onyo lake dhidi ya kuchanganya siasa na muziki, limewasha moto na sasa anashambuliwa nje ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na wasanii ambao wanasema ni jambo lisilowezekana kutofautisha mawili hayo.

Dk Mwakyembe, ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuchukua nafasi ya Nape Nnauye aliwataka wasanii kuachana na nyimbo zinazoishambulia Serikali au viongozi na kuwataka wachague ama kuwa wasanii au wanasiasa.

Alikuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule, ambaye pia ni mwanamuziki wa rap akijulikana kwa jina la Profesa J, kuwa wasanii wanaoiimba nyimbo za siasa kuihoji Serikali wamekuwa wakinyanyaswa. Dk Mwakyembe alisema wakati akijibu swali hilo kuwa wasanii waelekeze tungo zao kwenye burudani si siasa. Juzi, mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi, ambaye kisanii anajulikana kama Sugu, alisema imefika wakati kwa Dk Mwakyembe kujiwekea utaratibu wa kusoma na kufanya tafiti za kina kabla ya kutoa kauli ambazo hazitekelezeki.

Alisema kumpangia mwanamuziki atunge au aimbe nini, ni jambo lisilowezekana kwa kuwa tungo nyingi ni zao la maisha halisi ya jamii ambayo mwanamuziki husika anatokea.

“Sitashangaa kusikia kauli hiyo imetenguliwa. Hili ni jambo la ajabu ndiyo sababu limetushangaza wengi. Muziki ndiyo silaha ya kwanza ya ukombozi na haiwezekani kumpangia mwanamuziki atunge au aimbe kuhusu nini,” alisema Sugu ambaye aliibuka kwa kuimba nyimbo za rap zenye ujumbe wa siasa.

“Inawezekana vipi tu juzi aseme kuwa Rais ameruhusu wimbo wa Nay (wa Mitego) upigwe redioni na kusisitiza kuwa yupo huru atunge nyimbo nyingine, halafu leo anakuja kusema kuwa mwanamuziki asiimbe nyimbo za siasa? Ndiyo sababu nina imani kauli hii nayo itakuja kufutwa,” alisema Mbilinyi.

Hoja hiyo haikuwa tofauti sana na iliyotolewa na mwanamuziki kutoka kundi la Weusi, Nikki wa Pili aliyesema kuwa sanaa ni mali ya msanii na mara zote anaimba kutokana na uzoefu wake wa kile kinachoendelea kwenye jamii.

Alisema licha ya kuwapo kwa mgongano wa muda mrefu kati ya Serikali na sanaa, ni vigumu kutenganisha siasa na sanaa kwa kuwa vimekuwa vikishirikishana.

“Sanaa imekuwa ikitumika kufanya harakati za ukombozi na siasa. Hakuna namna ambavyo unaweza kuzuia sanaa isiingie kwenye siasa kwa kuwa ina mchango mkubwa upande huo. Naweza kusema sanaa na siasa ni mapacha wa miaka mingi,” alisema Nikki.

Kauli kama hiyo ilitolewa na Nay wa Mitego, ambaye aliwahi kukamatwa kwa wimbo wake wa “Wapo”, aliyesema muziki na siasa ni maisha ya mwanadamu.

“Nadhani waziri mwenyewe atakuwa na majibu ya kina kuhusu alichokisema. Huenda ana nia njema ya kutuepusha vijana wake kwenye hatari kwa mujibu wa hali anavyoiona. Ila binafsi naamini naimba muziki unaogusa maisha halisi ya jamii niliyopo,” alisema.

Muigizaji wa filamu Shamsa Ford alisema kauli hiyo ya waziri inalenga kuwanyima haki wasanii kushiriki kwenye siasa ilhali nao ni sehemu ya jamii.

“Msanii naye ana haki ya kupiga kelele kwa masilahi ya Taifa lake. Anapoona jambo haliendi sawa ni jukumu lake kupaza sauti, kwa nini tuzuiwe. Kama hufanyi uchochezi sioni sababu ya kuwekewa mipaka,” alisema Shamsa.

Rais wa Shirikisho la Filamu nchini (Taff), Simon Mwakifwamba alisema ipo haja ya sanaa kuangaliwa kwa mapana yake kwa kuwa ina nafasi ya kujenga au kubomoa jamii.     

BAADA YA CHIBU PERFUME ..ALIKIBA ATANGAZA BIDHAA ATAZOLETA

Habari njema za Mastaa wa bongo kutengeneza njia za kujiongezea kipato zaidi kwa kutengeneza bidhaa zenye majina yao zinaendelea kuongezeka ambapo leo ni zamu ya Alikiba.
Zikiwa zimepita wiki mbili toka Mwimbaji mwingine staa wa Bongofleva Diamond Platnumz kuzindua Perfume yake, leo May 11, 2017 kupitia 255 ya XXL Mwimbaji staa wa ‘aje’ Alikiba ameweka wazi kuwa moja ya mipango yake ni kutoa mavazi aina ya jeans, miwani, viatu na vinywaji vya energy vyenye jina lake.

Alikiba amesema kuwa hiyo ni mipango mizito na hatarajii kuifanya kiholela kwani hata mwanzo alifanya kama promotion lakini sasa hivi hayupo tayari kuikosea serikali na amejipanga kufungua na duka ili watu wake waweze kupata kwa urahisi.

“AK ni Brand ya Alikiba nashukuru imekuwa kubwa watu wanavaa lakini pia ipo na ya King Kiba nayo ni brand yangu na zipo official kabisa na kazi zitakapoanza watapata product zote’ – Alikiba

“Kuna Malengo makubwa sana tumeyaweka lakini siwezi kusema sasa hivi ila kuna Jeans Viatu na Glasses tayari zishatoka soon wataziona maana hizi zitakuwa za kwanza sababu tayari zishatoka na kuna energy drink” – Alikiba

RAIS MPYA MOON JAE-IN WA KOREA KUSINI APANGUA VIONGOZI

Lee Nak-yon, Mkuu wa Mkoa wa Jeolla Kusini, ametajwa kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Rais Moon. Uteuzi wake utawasilishwa katika Bunge la nchi hiyo na ataanza kutekeleza majukumu yake baada ya kupitishwa na wabunge.
Korea Kusini. Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini aliyechaguliwa juzi, amefanya mabadiliko makubwa katika safu ya uongozi akiwateua waziri mkuu mpya, mkuu wa shirika la ujasusi, mnadhimu mkuu wa Ikulu na mkuu wa huduma ya usalama wa Rais. 

Lee Nak-yon, Mkuu wa Mkoa wa Jeolla Kusini, ametajwa kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Rais Moon. Uteuzi wake utawasilishwa katika Bunge la nchi hiyo na ataanza kutekeleza majukumu yake baada ya kupitishwa na wabunge.@ 

Rais Moon pia amemteua Im Jong-seok kuwa Mnadhimu Mkuu wa Ikulu, huku Suh Hoon akiteuliwa kuchukua wadhifa wa mkuu wa shirika la ujasusi la Korea Kusini.

POLISI WAFANYA UKAGUZI WA MAGARI YA SHULE 

Ukaguzi huo ambao umeanza leo (Alhamisi) unasimamiwa na Kamanda wa Usalama Barabarani mkoani hapa, mhandisi Nuru Seleman na unalenga kuhakikisha hakuna gari bovu ambalo litaruhusiwa kuwa barabarani.
Polisi Mkoa wa Arusha wameanza ukaguzi wa magari yote ya shule ili kubaini kama ni mazima.

Ukaguzi huo ambao umeanza leo (Alhamisi) unasimamiwa na Kamanda wa Usalama Barabarani mkoani hapa, mhandisi Nuru Seleman na unalenga kuhakikisha hakuna gari bovu ambalo litaruhusiwa kuwa barabarani.

Hata hivyo, Seleman alishauri wamiliki wa magari wote mkoani Arusha wafuate sheria kuhakikisha magari yanabeba watu kulingana na uwezo wake ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa magari yao.

NYUMBA 9,500 ZA ASKARI MAGEREZA KUJENGWA

Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akishirikiana na Viongozi wengine kufungua Gereza la Wanawake wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.
Akizungumza leo (Alhamisi) wakati wa uzinduzi wa gereza la wanawake wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,  Hamad Masauni amesema Serikali inatambua changamoto za makazi ya askari Magereza na tayari iko katika mazungumzo na benki ya Exim ili iweze kujenga nyumba hizo.

Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Exim inatarajia kujenga nyumba 9,500 za askari Magereza ili kukabiliana na changamoto za makazi ya askari wa jeshi hilo nchini.

Akizungumza leo (Alhamisi) wakati wa uzinduzi wa gereza la wanawake wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,  Hamad Masauni amesema Serikali inatambua changamoto za makazi ya askari Magereza na tayari iko katika mazungumzo na benki ya Exim ili iweze kujenga nyumba hizo.

“Nawaomba askari wetu nchi nzima  wawe na subira, Serikali inatambua pia inashughulikia changamoto ya makazi ya  askari na tayari tuko katika mazungumzo na wadau, ikiwemo benki ya Exim kuanza mradi wa ujenzi wa nyumba takriban 9,500,”amesema.

Awali, akitoa maelezo ya ujenzi wa gereza hilo uliogharimu Sh65 milioni, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Dk Juma Malewa amesema ujenzi wa gereza hilo umefanywa na wataalamu ambao ni askari Magereza kwa  kushirikiana na wafungwa kama sehemu ya utekelezaji wa  agizo la Rais John Magufuli la kutaka wafungwa watumike katika kazi za uzalishaji ikiwemo kilimo, ujenzi na ufundi.

Dk Malewa amesema gereza hilo litasaidia  kuhifadhi wafungwa 148 na hivyo kupunguza msongamano wa wafungwa katika gereza la Kongwa.

JPM AMWOMBA RAIS ZUMA AKAMPIGIE DEBE KWA AJILI YA KUPATA MKOPO

Rais John Magufuli amemwomba Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini,ampigie debe kwenye jumuiya ya BRICKS kwa ajili ya kupata  mkopo wa kuendeleza ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) kutoka Morogoro hadi Dodoma.
Rais Magufuli ambaye hakutaja kiasi cha mkopo huo, ametoa ombi hilo leo (Alhamisi) wakati wa hafla ya kutia saini mikataba ya ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hiyo.

Amemwambia Rais Zuma kuwa hivi sasa Serikali ya Tanzania ina fedha za kujenga reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, hivyo fedha zaidi zinahitajika kwa ajili ya kuendeleza ujenzi kutoka Morogoro hadi Dodoma.

Rais Magufuli amesema anaamini Serikali ya Afrika Kusini itasaidia ombi hilo kwa kuwa ni mwanachama mzuri wa jumuiya hiyo na pia Tanzania na Afrika Kusini zimekuwa na historia nzuri .

TANZANIA,AFRIKA KUSINI KUONGEZA MAENEO YA BIASHARA NA UWEKEZAJI

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,  Balozi Augustine Mahiga amesema Serikali za Tanzania na Afrika Kusini zimeweka mikakati ya kuongeza maeneo ya ushirikiano, hususan katika biashara na uwekezaji.
Balozi Mahiga amesema hayo leo (Alhamisi) asubuhi alipotoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa mawaziri wa kamisheni ya pamoja ya kitaifa kati ya Tanzania na Afrika Kusini uliofanyika jijini hapa.

Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini,  Maite Nkoana -Mashabane ameeleza umuhimu wa kukuza uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya mataifa hayo mawili ili kuwaletea maendeleo wananchi wa mataifa yote.

Pia, ametumia fursa hiyo kutoa rambirambi kwa Tanzania kwa vifo vya watoto 32, walimu wawili na dereva mmoja wa Shule ya Lucky Vincent vilivyotokea wiki iliyopita mkoani Arusha. Amesema ajali imepunguza nguvu kazi na wataalamu wa kizazi kijacho.